Makala
KITABU CHA ZABURI
| Makala
ZABURI:
Day 02
MLANGO 6
Bwana, usinikemee kwa hasira yako, Wala usinirudi kwa ghadhabu yako.
2 Bwana, unifadhili, maana ninanyauka; Bwana, uniponye, mifupa yangu imefadhaika.
3 Na nafsi yangu imefadhaika sana; Na Wewe, Bwana, hata lini?
4 Bwana urudi, uniopoe nafsi yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
5 Maana mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru?
6 Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakieleza kitanda changu; Nalilowesha godoro langu kwa machozi yangu.
7 Jicho langu limeharibika kwa masumbufu, Na kuchakaa kwa sababu yao wanaoniudhi.
8 Ondokeni kwangu, ninyi nyote mtendao uovu; Kwa kuwa Bwana ameisikia sauti ya kilio changu.
9 Bwana ameisikia dua yangu; Bwana atayatakabali maombi yangu.
10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika.
MLANGO 7
Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
2 Asije akaipapura nafsi yangu kama simba, Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya.
3 Bwana, Mungu wangu, ikiwa nimetenda haya, Ikiwa mna uovu mikononi mwangu,
4 Ikiwa nimemlipa mabaya Yeye aliyekaa kwangu salama; (Hasha! Nimemponya yeye Aliyekuwa mtesi wangu bila sababu;)
5 Basi adui na anifuatie, Na kuikamata nafsi yangu; Naam, aukanyage uzima wangu, Na kuulaza utukufu wangu mavumbini.
6 Bwana uondoke kwa hasira yako; Ujiinue juu ya jeuri ya watesi wangu; Uamke kwa ajili yangu; Umeamuru hukumu.
7 Kusanyiko la mataifa na likuzunguke, Na juu yake uketi utawale.
8 Bwana atawaamua mataifa, Bwana, unihukumu mimi, Kwa kadiri ya haki yangu, Sawasawa na unyofu nilio nao.
9 Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki.
10 Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo.
11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.
12 Mtu asiporejea ataunoa upanga wake; Ameupinda uta wake na kuuweka tayari;
13 Naye amemtengenezea silaha za kufisha, Akifanya mishale yake kuwa ya moto.
14 Tazama, huyu ana utungu wa uovu, Amechukua mimba ya madhara, amezaa uongo.
15 Amechimba shimo, amelichimba chini sana, Akatumbukia katika handaki aliyoifanya!
16 Madhara yake yatamrejea kichwani pake, Na dhuluma yake itamshukia utosini.
17 Nitamshukuru Bwana kwa kadiri ya haki yake; Nitaliimbia jina la Bwana aliye juu.
MLANGO 8
Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;
2 Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao Umeiweka misingi ya nguvu; Kwa sababu yao wanaoshindana nawe; Uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.
3 Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, Mwezi na nyota ulizoziratibisha;
4 Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie?
5 Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima;
6 Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
7 Kondoo, na ng'ombe wote pia; Naam, na wanyama wa kondeni;
8 Ndege wa angani, na samaki wa baharini; Na kila kipitacho njia za baharini.
9 Wewe, MUNGU, Bwana wetu, Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
MLANGO 9
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote; Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;
2 Nitafurahi na kukushangilia Wewe; Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu.
3 Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako.
4 Kwa maana umenifanyia hukumu na haki Umeketi kitini pa enzi ukihukumu kwa haki.
5 Umewakemea mataifa; Na kumwangamiza mdhalimu; Umelifuta jina lao milele na milele;
6 Adui wamekoma na kuachwa ukiwa milele. Nayo miji yao uliing'oa; Hata kumbukumbu lao limepotea.
7 Bali Bwana atakaa milele, Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu.
8 Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki; Atawaamua watu kwa adili.
9 Bwana atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida.
10 Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, Bwana hukuwaacha wakutafutao.
11 Mwimbieni Bwana akaaye Sayuni, Yatangazeni kati ya watu matendo yake.
12 Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka, Hakukisahau kilio cha wanyonge.
13 Wewe, Bwana, unifadhili, Tazama mateso niteswayo na wanaonichukia; Wewe uniinuaye katika malango ya mauti,
14 Ili nizisimulie sifa zako zote; Katika malango ya binti Sayuni Nitaufurahia wokovu wako.
15 Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya; Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao.
16 Bwana amejidhihirisha na kutekeleza hukumu; Amemnasa mdhalimu kwa kazi ya mikono yake.
17 Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.
18 Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima; Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele.
19 Bwana, usimame, mwanadamu asipate nguvu, Mataifa wahukumiwe mbele zako.
20 Bwana, uwawekee kitisho, Mataifa na wajijue kuwa ni binadamu.
MLANGO 10
Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?
2 Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.
3 Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.
4 Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Hatapatiliza. Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu;
5 Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awafyonya.
6 Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni.
7 Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,
8 Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni.
9 Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake.
10 Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake.
11 Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe.
12 Bwana, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge.
13 Kwani mdhalimu kumdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza?
14 Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima.
15 Uuvunje mkono wake mdhalimu, Na mbaya, uipatilize dhuluma yake, hata usiione.
16 Bwana ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa wamepotea kutoka nchi yake.
17 Bwana, umeisikia tamaa ya wanyonge, Utaitengeneza mioyo yao, utalitega sikio lako.
18 Ili kumhukumu yatima naye aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.
SADAKA