KUSOMA KITABU CHA ZABURI {SEHEMU YA 04}

| Makala

KUSOMA KITABU CHA ZABURI:

                          Day 04:

Zaburi 16

1  Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe.

2  Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; Sina wema ila utokao kwako.

3  Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao.

4  Huzuni zao zitaongezeka Wambadilio Mungu kwa mwingine; Sitazimimina sadaka zao za damu, Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu.

5  Bwana ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu.

6  Kamba zangu zimeniangukia mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri.

7  Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.

8  Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.

9  Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nao utukufu wangu unashangilia, Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.

10  Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.

11  Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.


 

Zaburi 17

1  Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.

2  Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili.

3  Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose,

4  Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.

5  Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.

6  Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu.

7  Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.

8  Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;

9  Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka.

10  Wameukaza moyo wako, Kwa vinywa vyao hutoa majivuno.

11  Sasa wametuzunguka hatua zetu, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini.

12  Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwana-simba aoteaye katika maoteo yake.

13  Ee Bwana, usimame, umkabili, umwinamishe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi na mtu mbaya.

14  Ee Bwana, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao li katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao,

15  Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.


 

Zaburi 18

1  Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;

2  Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.

3  Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu.

4  Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.

5  Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili.

6  Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.

7  Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu.

8  Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala, Makaa yakawashwa nao.

9  Aliziinamisha mbingu akashuka, Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake.

10  Akapanda juu ya kerubi akaruka, Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo.

11  Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha, Kuwa hema yake ya kumzunguka. Giza la maji na mawingu makuu ya mbinguni.

12  Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Kukapita mawingu yake makuu. Mvua ya mawe na makaa ya moto.

13  Bwana alipiga radi mbinguni, Yeye Aliye juu akaitoa sauti yake, Mvua ya mawe na makaa ya moto.

14  Akaipiga mishale yake akawatawanya, Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya.

15  Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee Bwana, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.

16  Alipeleka kutoka juu akanishika, Na kunitoa katika maji mengi.

17  Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.

18  Walinikabili siku ya msiba wangu, Lakini Bwana alikuwa tegemeo langu.

19  Akanitoa akanipeleka panapo nafasi, Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.

20  Bwana alinitendea sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa.

21  Maana nimezishika njia za Bwana, Wala sikumwasi Mungu wangu.

22  Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu, Wala amri zake sikujiepusha nazo.

23  Nami nalikuwa mkamilifu mbele zake, Nikajilinda na uovu wangu.

24  Mradi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.

25  Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;

26  Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi.

27  Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili.

28  Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu; Bwana Mungu wangu aniangazia giza langu.

29  Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi, Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta.

30  Mungu, njia yake ni kamilifu, Ahadi ya Bwana imehakikishwa, Yeye ndiye ngao yao. Wote wanaomkimbilia.

31  Maana ni nani aliye Mungu ila Bwana? Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu?

32  Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu.

33  Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.

34  Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba.

35  Nawe umenipa ngao ya wokovu wako, Mkono wako wa kuume umenitegemeza, Na unyenyekevu wako umenikuza.

36  Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Na miguu yangu haikuteleza.

37  Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala sitarudi nyuma hata wakomeshwe.

38  Nitawapiga-piga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu.

39  Nawe hunifunga mshipi wa nguvu kwa vita, Hunitiishia chini yangu walioniondokea.

40  Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Nao walionichukia nimewakatilia mbali.

41  Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa, Walimwita Bwana lakini hakuwajibu,

42  Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo, Nikawatupa nje kama matope ya njiani.

43  Umeniokoa na mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia.

44  Kwa kusikia tu habari zangu, Mara wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea.

45  Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka.

46  Bwana ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu;

47  Ndiye Mungu anipatiaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu.

48  Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu wa jeuri.

49  Basi, Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako.

50  Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi


 

Zaburi 19

1  Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.

2  Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa.

3  Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani.

4  Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema,

5  Kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake.

6  Kutoka kwake lautoka mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake hata miisho yake, Wala kwa hari yake Hakuna kitu kilichositirika.

7  Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.

8  Maagizo ya Bwana ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya Bwana ni safi, Huyatia macho nuru.

9  Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa.

10  Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali.

11  Tena mtumishi wako huonywa kwazo, Katika kuzishika kuna thawabu nyingi.

12  Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri.

13  Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa.

14  Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.


 

Zaburi 20

1  Bwana akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue.

2  Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni.

3  Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako.

4  Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.

5  Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. Bwana akutimizie matakwa yako yote.

6  Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi

7  Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.

8  Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.

9  Bwana, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo.


 SADAKA