MIDOMO YA MALAYA INAYODONDOZA ASALI

| Makala

MITHALI SURA YA 5:

Mithali hii inaendelea kutoa maonyo juu ya uharibifu unaotokana na uasherati/uzinzi.

Suleimani aliyeandika kitabu hiki,anasisitiza kuwa - ingawa upotovu wa maadili hudanganya na kuonyesha mambo mazuri ya kuvutia,kujiingiza katika matendo hayo kutasababisha maangamizo.

Kukiuka viwango vya Mungu kuhusu usafi kuhusu usafi wa mahusiano kijinsia na kutunza maisha yetu ni vitu vinavyopatikana katika sura hii ya 5 ya kitabu cha mithali.

Njia pekee ya kuepuka mambo haya ni kujiweka kwa Mungu,kujiadabisha na kujizuia kabla ya ndoa,na kutosheleza shauku ya asili ya tendo la ndoa kwa njia ya maisha ya upendo mtakatifu katika ndoa.

Mungu ameamua kuwa wale wanaojiingiza kwenye tamaa za mwili watapata majuto kutokana na kuharibika kwa maisha ya kifamilia na watateseka katika maisha yao.Kumbuka haya ni maamuzi ya Mungu mwenyewe kwa kila atakayekiuka maelekezo haya.

Tendo la ndoa kabla ya ndoa,na kutokuwa mwaminifu katika ndoa - huleta maangamizi.Maana lile lianzalo kama utamu,humalizika na uchungu.

Mahusiano mengi yameharibika na ndoa nyingi zimevunjika kwa sababu ya kukosa maarifa kama haya ya HEKIMA ya Mungu katika kutunza mahusiano na ndoa yako.

Uzinzi na Uasherati ni dhambi mbili kubwa ambazo shetani anazitumia sana katika kuangamiza hatma za watu na kuharibu kabisa maisha yao.{sexual immorality and adultery}

Haya mambo ya kuchochea uzinzi na uasherati yamepamba moto sana kwa majira tuliyonayo,na ndio njia kubwa sana na mtego wa maana kwa shetani kuvuna watu ili awaharibie maisha yao,na pia awapate wa kwenda nao jehanam kwenye ziwa la moto.

Channel za TV zinachochea uzinzi,mitandaoni ndio usiseme kabisa,majarida mbalimbali,wengine wameamua kabisa kufanya biashara ya miili yao tena kwa bei za ajabu sana sababu wameshindwa kujiona kuwa wao ni wa thamani na hawatakiwi kushiriki biashara hiyo chafu.

Na sikuhizi hii biashara ya watu,mpaka delivery ipo {usiniulize nimejuaje!!!!}.

Yaani dunia kwa sasa imeonyesha kuwa uovu huu wa uzinzi ni jambo la kawaida sana sana sana,na halina madhara.Yaani ni kama kula tu Ice Cream.

Uzinzi ni moja kati ya muuaji mkubwa wa hatma za watu. Sawasawa na neno la mungu linasema kuwa “mshahara wa dhambi ni mauti”

Uzinzi na uashetani huiba furaha ya mtu,huangamiza familia mbalimbali na pia hata maisha ya wengine huathirika kabisa.Biblia inatuonya kwenye Mithali 5:5 kuwa “miguu ya mzinzi huteremika mauti,na hatua zake zinashikamana na kuzimu”

Uzinzi sio dhambi ya kufanya bahati mbaya, na pia sio dhambi ya kukaa na kujadili kuwa utashinda jaribu hilo….biblia inasema kuwa “IKIMBIE ZINAA” na biblia ikisema kimbia,inamaanisha KIMBIA kweli kweli.

Mungu hadhihakiwi,unachokipanda leo utakivuna kesho.


USHAURI MUHIMU WA KUZINGATIA:

=> Usikubali kuilisha akili yako kupitia television,movies,vitabu visivyofaa nk vilivyobeba maudhui ya uzinzi na uasherati,kwa maana kile unachojilisha leo kwenye ufahamu wako - unaweza usione matokeo ya haraka leo leo lakini kesho yako utatamani kutoka na haitawezekana kabisa,maana utakuwa umezama kwenye shimo alilokuwa amekutegea shetani bila wewe kujua.

Muheshimu Mungu,jiheshimu na wewe pia, kwa kufanya hivyo - itakusaidia kuwaheshimu na wengine pia.


+255 758 708804 

Pastor Dr Innocent Mashauri

Mshauri wa mambo ya kiroho {Spiritual Advisor} kwa njia ya Neno la Mungu na Maombi.

Madhabahu ya SIRI ZA BIBLIA

[MAARIFA YA KI-MUNGU]


 SADAKA