Makala
SOMA HAPA KITABU CHA ZABURI: DAY 03
| Makala
MLANGO 11
Bwana ndiye niliyemkimbilia. Mbona mnaiambia nafsi yangu, Kimbia kama ndege mlimani kwenu?
2 Maana, tazama, wasio haki wanaupinda uta, Wanaitia mishale yao katika upote, Ili kuwapiga gizani wanyofu wa moyo.
3 Kama misingi ikiharibika, Mwenye haki atafanya nini?
4 Bwana yu katika hekalu lake takatifu. Bwana ambaye kiti chake kiko mbinguni, Macho yake yanaangalia; Kope zake zinawajaribu wanadamu.
5 Bwana humjaribu mwenye haki; Bali nafsi yake humchukia asiye haki, Na mwenye kupenda udhalimu.
6 Awanyeshee wasio haki mitego, Moto na kiberiti na upepo wa hari, Na viwe fungu la kikombe chao.
7 Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye haki, Apenda matendo ya haki, Wanyofu wa moyo watamwona uso wake.
MLANGO 12
Bwana, uokoe, maana mcha Mungu amekoma, Maana waaminifu wametoweka katika wanadamu.
2 Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe, Wenye midomo ya kujipendekeza; Husemezana kwa mioyo ya unafiki;
3 Bwana ataikata midomo yote ya kujipendekeza, Nao ulimi unenao maneno ya kiburi;
4 Waliosema, Kwa ndimi zetu tutashinda; Midomo yetu ni yetu wenyewe, Ni nani aliye bwana juu yetu?
5 Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge, Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, Sasa nitasimama, asema Bwana, Nitamweka salama yeye wanayemfyonya.
6 Maneno ya Bwana ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.
7 Wewe, Bwana, ndiwe utakayetuhifadhi, Utatulinda na kizazi hiki milele.
8 Wasio haki hutembea pande zote, Ufisadi ukitukuka kati ya wanadamu.
MLANGO 13
Ee Bwana, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako?
2 Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?
3 Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti.
4 Adui yangu asije akasema, Nimemshinda; Watesi wangu wasifurahi ninapoondoshwa.
5 Nami nimezitumainia fadhili zako; Moyo wangu na uufurahie wokovu wako.
6 Naam, nimwimbie Bwana, Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu.
MLANGO 14
Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema.
2 Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu.
3 Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.
4 Je! Wote wafanyao maovu hawajui? Walao watu wangu kama walavyo mkate, Hawamwiti Bwana.
5 Hapo ndipo walipoingiwa na hofu nyingi, Maana Mungu yupo pamoja na kizazi cha haki.
6 Mnalitia aibu shauri la mtu mnyonge, Bali Bwana ndiye aliye kimbilio lake.
7 Laiti wokovu wa Israeli utoke katika Sayuni! Bwana awarudishapo wafungwa wa watu wake; Yakobo atashangilia, Israeli atafurahi.
MLANGO 15
Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu?
2 Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, Na kutenda haki. Asemaye kweli kwa moyo wake,
3 Asiyesingizia kwa ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, Wala hakumsengenya jirani yake.
4 Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana Ingawa ameapa kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake.
5 Hakutoa fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.
SADAKA